MSALA Sehemu Ya Kwanza-01

 

Hadithi za kiswahili Msala

MSALA Sehemu Ya Kwanza-01


MSALA

Naitwa Benjamin Kingai, Mimi ni Rubani wa Ndege za shirika la Air Tornado. Nilikutana na Mkasa kwenye Maisha yangu, Mkasa ambao sitokuja kuusahau hadi naingia kaburini, Nakumbuka ilikua ni Jumamosi.


Nilienda Arusha kwa Mpenzi wangu ili Jumatatu niingie Kazini, hivyo Jumapili Usiku nilianza safari ya kurudi Dar-es-salaam, mara nyingi napendelea kufanya safari Usiku wakati magari yamepungua sana. Sasa Usiku wa Jumapili nikiwa ndani ya gari yangu aina ya Toyota TX nilikutana na Msichana mmoja nisiyemfahamu akiwa anakimbizwa na Watu waliovalia Mask Usoni akitokea Msituni, sikumjua yule Msichana lakini namna alivyokua akinipungia nimsaidie ilinihamasisha sana nikajikuta haraka nafunga Breki na kumsaidia.


Yule Msichana alikua na majeraha kadhaa ya visu, damu nyingi ilikua imemtoka. Alikua na maumivu makali kila sehemu.


Kabla sijamuuliza chochote niliiyona gari ikija kwa kasi sana nyuma yetu, haraka nilihisi huwenda Wale Watu waliokua wakimfukuzia walikua wanakuja, nikaongeza spidi, kwa hali ya yule Msichana ilihitaji matibabu ya Haraka sana ili kuokoa Uhai wake, nilijikuta ndani ya Kisa nisichokijua kimeanzia wapi wala kinaenda kuishia wapi.


Nilijitahidi kukimbizana na lile gari lililo nyuma yetu hadi tunafika Chalinze, ilikua Mishale ya saa saba Usiku, nikaliingiza gari mahali penye Watu, lile gari ndogo likatupita na kwenda kusimama mbele kidogo likitusubiria.


Watu waliokua pale Chalinze stendi muda huo walikua ni wale wasio na mahali pa kulala hivyo mara nyingi hukesha wakizungumza, haraka sikuona kama wanaweza kua Msaada kwangu, lile gari lilikua limesimama likitusubiria. Yule Msichana alikua amevuja damu nyingi, alikua hawezi kuongea chochote, nilifikiria zaidi kuhusu uhai wake lakini namna ya kumsaidia ilikua Mtihani sana kwangu


Nilivuta simu yangu ili nitafute Msaada kwa Watu ninaowajua, wengi hawakupokea simu yangu, ikawa Mtihani sana kwangu kuchomoka Chalinze, giza lilikua limeshamiri lakini kupitia taa ya gari niliimurika ile gari yenye vioo vyeusi, sikumwona yeyote yule ndani ya gari kutokana na Aina ya vioo vya gari.


Nilitia gia, nilivuta pumzi zangu, nikaliingiza tena lile gari Barabarani, macho yangu yalikua kwenye kioo cha gari langu kuona kama Wale Watu walikua wakija, lile gari pia lilianza kutembea myuma yetu, ikanipa uhakika kabisa kua Walikua wakitufukuzia sisi, moyoni nilijiuliza yule Msichana alifanya jambo gani hadi afukuzwe namna ile


***


Sikumjua yule Msichana alikua Nani, lakini mavazi yake yalinifanya nimtafsri kwa haraka haraka nikiwa nakanyaga Mafuta, alivalia gauni fupi sana lenye Mg’ao, chini hakua na kiatu pengine labda alivitupa wakati anafukuzwa. Kichwani alivalia wigi fupi lenye nywele za kahawia, alibandika kucha pia alikua na Kope Machoni pake.


Sijui niliwezaje kugundua katika mazingira yale ya Purukushani kua alikua na Lenzi machoni pake, vyote niliona kama Urembo tu. Nilihisi pengine labda aligonganisha Wanaume alipokua kwenye Mtoko lakini hisia zangu hazikunipa uhakika zaidi kwani nilijiuliza alifikaje kule msituni na giza lile, Watu wale walidhamiria kummaliza


Mshale wa mafuta ndani ya gari yangu ulikua unazidi kunikatisha tamaa, sijui ni kwanini Usiku ule sikujaza mafuta ya kutosha wakati natoka Arusha, siku ya Msala haikwepeki, gari iliyo nyuma yetu nilifanikiwa kuifahamu ilikua ni Kulger, kwa uwezo wa gari isingeliweza kufua dafu mbele ya Toyota TX lakini namna ilivyokua inaendeshwa ilinifanya nigundue kua dereva alikua fundi haswa wa kuendesha gari.


Yule Msichana alikua akitapatapa kwa Maumivu makali huku damu zikizidi kumvuja, eneo tulilopo halikuwa na taa yoyote iliyoonesha palikua na makazi ya Watu, tulizungukwa na Msitu kila Upande


“Wewe ni Nani?” nilimuuliza kwa mara ya kwanza swali hili, nilishindwa kuvumilia kumsaidia Mtu nisiyemjua, nikiweka Maisha yangu rahani kwa ajili yake bila kukusudia


“Elizabeth Mlacha” alisema huku akigugumia kwa maumivu makali, sikutaka kuendelea kupoteza muda nilimtupia swali la pili huku nikizidi kukanyaga mafuta.


“Kwanini wanakufukuza?” ile hali ilinifanya nichanganikiwe, hata namna nilivyokua naongea nilikua katika hofu kubwa sana.


“They want to Kill Me, wametumwa wanimalize” alisema kwa sauti ya juu huku chozi likimbubujika, nilitafakari kwanini watake kumuuwa, kabla sijamuuliza Risasi ilipigwa kwenye kioo ikanikwaruza Begani, nikayumba na lile gari lakini niliweza kuhimili kuliweka sawa Barabarani, niliiyona hali ya hatari mbele yangu, nilijuta kwanini nilimsaidia yule Msichana.


“Shit” nilisema nikiwa natumia mkono mmoja pekee kuliongoza lile gari maana mkono ambao nilijeruhiwa Bega ulikua unapoteza nguvu taratibu


“Ni Nani wale?” nilimuuliza huku nikijitahidi kukwepesha uelekeo wa gari ili kama kuna risasi itapigwa tena isitupate, nikawa naiyumbisha


“Wauwaji wa kuaminika, wametumwa na……..” kabla hajamaliza kuzungumza, tairi za gari zilipasuka ghafla tukiwa katikati ya Barabara, risasi zilizopigwa kwa mara ya pili zililenga Matairi, gari ilinishinda nikajikuta nikiiruhusu kuzama kwenye Korongo refu, gari ilivingirika zaidi ya mara sita kisha ikaenda kukita kwenye Mti na kukaa sawa. 


Moshi ukafuka, Kichwa changu kikawa kinapiga kelele ya Kuchanganikiwa, nikawa nasikia sauti za filimbi, nilipata jeraha eneo la kichwa, damu ilikua ikinivuja. Bahati nzuri ndani ya sekunde kadhaa akili yangu ilirejea katika ufahamu wa kawaida, nikavunja kioo cha gari ambacho kilikua kimejenga ufa kama utando wa Buibui hivyo hakikunipa fursa ya kuona chochote nje ya Gari


Nilipovunja niliwaona Wanaume watatu wakiwa wanateremka kuja mahali ambako sisi tuliangukia, palikua na umbali kidogo kwa namna gari ilivyokua imevingirika. Nilimtazama yule Msichana aliyejitambukisha kwangu kama Elizabeth Mlacha.


Alikua hajitambui lakini alikua akisema


“Usiniache wataniuwa” Kwanza nilijisaidia nikatoka ndani ya lile gari kisha nikasogea upande wa mlango ambao Elizabeth alikuwepo, nilijaribu kuufungua lakini ulikua umeshajibamiza na mfumo mzima wa Mlango huo ulivurugika hivyo mlango uligoma kufunguka, tochi zikawa zinakuja karibu na tulipo, bado Elizabeth alikua ndani ya lile gari. Nini kitaendelea? Usikose sehemu ya Pili 

Previous Post Next Post

نموذج الاتصال