MSALA Sehemu Ya Pili-02
MSALA
Ilipoishia “Usiniache wataniuwa” Kwanza nilijisaidia nikatoka ndani ya lile gari kisha nikasogea upande wa mlango ambao Elizabeth alikuwepo, nilijaribu kuufungua lakini ulikua umeshajibamiza na mfumo mzima wa Mlango huo ulivurugika hivyo mlango uligoma kufunguka, tochi zikawa zinakuja karibu na tulipo, bado Elizabeth alikua ndani ya lile gari.”
Endelea
SEHEMU YA PILI
Haraka nikarejea upande niliotokea kisha nikamvuta Elizabeth kwa nguvu na kufanikisha kumtoa ndani ya lile gari halafu nikambeba Mgongoni na kuanza kuchanja naye Mbuga Usiku huo. Sikujua nilikua naelekea wapi lakini kitu cha kwanza kilikua usalama wa Maisha yetu.
Wale wanaume walipofika waligundua tumeshatoka ndani ya gari hivyo wakajitawanya kuanza kutusaka, tulizama ndani ya Pori lenye Miba na madimbwi ya Maji yenye tope zito sana, sijui eneo hilo lilikua linatumika kwa kazi gani, nilipofika umbali kidogo bahati mbaya niliterezea kwenye kisima kimoja
Elizabeth akawa anataka kutumbukia nikamdaka, nikawa namvuta haraka ili tuendelee na safari, Tochi ilikua ikija upande ule nilipokua namvuta Elizabeth, niliongeza spidi kumvuta hadi nikamfikisha juu, nikamvuta tena tukajificha kwenye kichaka kimoja.
Nilikua nahema kwa shida sana sababu nilikua na Ugonjwa wa pumu, ile baridi ilianza kuniathiri na kunifanya nianze kudhohofu. Nguvu zilianza kuniisha, macho yangu yaliona giza zaidi kuliko mwanga sababu eneo lile lilikua giza tupu, angalau yale madimbwi yalinisaidia kugundua kua kama kuna Mtu anakuja upande wetu
Walitusaka pale Porini kwa zaidi ya nusu saa tukiwa tumejibanza palepale kwenye kichaka, nilikua nahema kama Kuku mwenye Mdondo, Pumu ilinichukua kisawasawa. Dawa zangu za pumu zilikua ndani ya gari tuliyopata nayo ajali, kisha wale wanaume walikutana wote watatu wakisema
“Hawa hawapo mbali na hapa, kuna Mahali wamejificha. Ni lazima tuhakikishe tunawanasa kabla ya mapambazuko” alisema mmoja wao kwa sauti iliyokua imejaa mamlaka zaidi Msako ukaanza upya pale porini, wakatawanyika tena kutusaka
Nilimtikisa Elizabeth maana kwa jinsi nilivyokua na hali mbaya kwenye mfumo wa upumuaji isingeliweza kua rahisi kumbeba tena Elizabeth, nilishapata wazo la kurudi juu ya Barabara ili kutoroka na gari ya wale Wanaume waliozama zaidi porini, nilimtikisa sana Elizabeth lakini hakuamka.
Basi nikajikaza kiume japo nilikua na hali mbaya sana Kiafya, pumu ilizidi kunibana. Suluhu pekee ilikua ni dawa yangu iliyokua ndani ya gari, sikuona dalili yoyote ya Wale wanaume kurudi, nikapata wazo la haraka kwenda kuchukua dawa zangu kisha nimrudie Elizabeth.
Basi nikamwacha hapo nikawa najivuta taratibu kuelekea mahali lilipo gari, nilijivuta kwa shida, hadi nilipolifikia gari tulilopata nalo ajali, ndani yake ndimo ilimo dawa ya pumu, nilifungua Mlango wa gari kisha nikaichukua na kuipuliza mdomoni mwangu.
Taratibu hali yangu ilianza kukaa sawa, hapo hapo nikaanza kuona tochi zikimulika kuja upande niliopo, haraka nikazama uvunguni mwa lile gari ili kujificha wasinione. Mikanyago yao ilizidi kuja upande wangu hadi walipofika kwenye lile gari
“Tulipaswa kumuuwa Elizabeth kule Msituni, ni uzembe wako” wakaanza kulaumiana, nilijibana vizuri kuhakikisha hawanishtukii, lakini mmoja wao akasema
“Hebu tulieni, hamuhisi harufu fulani?” Yes!! Ilikua ni harufu ya ile dawa ya pumu niliyoitumia muda mchache uliopita, wote wakaivuta ile harufu.
“Mtu alikuwepo hapa, tumepoteza malengo” akasema Mmoja, nilianza kuingiwa na hofu maana kama Mmoja atachungulia chini ya gari huo utakua mwisho wa Maisha yangu, nilisali kwa jina la Baba na Mwana, nilimtaja Mungu wa Jacob anisaidie kwenye Kisanga kile.
Mmoja aliinamna na kuokota dawa ya pumu niliyokua nimeitumia
“Ndio Mtu alikua hapa muda Mchache uliopita” wakaanza kupekua lile gari na kukuta baadhi ya vitambulisho vyangu.
“Oooh!! Kumbe ni rubani wa ndege, tukimpata huyu tumempata Elizabeth, kwa jinsi ambavyo tumehangaika hapa Porini itakua wametupiga chenga ya Mwili na kutoweka” alisema Mmoja wao, haraka wakakimbilia juu, wakaingia kwenye gari na kushika Barabara inayoelekea Dar.
Nilichomoka uvunguni mwa Lile gari, nilifikiria sasa kumrudia Elizabeth pale Kichakani, nilifanya haraka kushuka hadi chini, nilianza kupapasia ni wapi nilipomwacha Elizabeth, giza lilikua totoro pale Porini, nilianza kuhangaika kumsaka Elizabeth bila Mafanikio, nilijaribu kumwita bila Mafanikio pia ya kuitikiwa.
Nilifkiria nifanye nini, tayari nilishaisahau sehemu ambayo nilimwacha Elizabeth, kibaya zaidi alikua amepoteza fahamu. Moyo wangu uliniambia haraka kua nikimbie eneo lile, halikua salama kabisa kwangu, lakini Moyo huo huo uliniuliza naondoka vipi bila ya yule Msichana?
Kama nitaondoka bila Msichana basi kazi niliyoifanya ya kuhatarisha Maisha yangu ingelikua ni sawa na Bure lakini nitampata vipi wakati nimesahau eneo nililomwacha, nikiwa katika tafakari hiyo nzito iliyotumia zaidi ya dakika moja, nilishtuka baada ya kumulikwa tochi kwa Mbali.
“Yule pale” ikasema sauti, sekunde hiyo hiyo gari moja ikasimama juu ya Barabara, sekunde ya tano Watu wakashuka na kuzama Porini, nilikua bado kitanzini nisijue nakimbilia wapi, jinsi Watu wenye tochi walivyokua wakishuka kule chini nilipo ilinifanya niduwae.
Walikua zaidi ya Watu kumi kwa makadirio ya Haraka Haraka, nilijiona ndani ya Bonde la Umauti, kila sekunde ilinuka harufu ya Kifo, Usiku huo ulikua Mgumu sana kwangu, ugumu ulisababishwa na kutokujua ni kwanini yule Msichana Elizabeth alikua akiandamwa namna ile, pili sikujua ni namna gani naweza kutoka salama
‘KIMBIA’ Nafsi yangu ilinishtuka haraka sana, nguvu ikanijaa nikageuka na kuanza kuzama porini nisijuwe naelekea sehemu gani, nilianza riadha ya haraka kusalimisha Maisha yangu maana walikua wameshaniona. Nilikimbia kwa spidi ya ajabu sana hata sijui ujuzi wa kuikimbiza roho yangu niliutolea wapi wakati hata Mazoezi nilikua sina.
Nililikata lile pori ili nipate msaada mbeleni lakini kadili nilivyokua nakimbia ndivyo nilivyoanza kuzama Msituni, nilijipiga kwenye Mti mmoja sababu nilikua sina tochi, giza lilikua la kutosha sana, sikujiuliza mara mbili kama nilikua nimeumia au nilikua salama, niliendelea kusonga mbele.
Nilifika mahali nikaamua kujificha maana tayari nilishachoka, nilijibanza nyuma ya Mti mmoja eneo ambalo lilikua limeshona miti midogo midogo iliyojitengeneza kama kichaka ndani ya Msitu huo, wale wanaume hawakuchukua dakika nyingi walifika nilipo huku wakiwa wanasema
“Kama hatutowapata basi tutakua tumejitoa kafara wenyewe” niliona wazi yule Msichana alikua Muhimu sana kwao, lakini sikuacha kujiuliza alikua ni Nani kwao, aliwafanya nini hadi watake kumuuwa. Mambo yashaanza kuwa makubwa sasa NINI KITAENDELEA? Usikose sehemu ya pili