MSALA Sehemu Ya Nane-08

 MSALA Sehemu Ya Nane-08

MSALA Sehemu Ya Nane-08
MSALA Sehemu Ya Nane-08


MSALA

Ilipoishia “Siku nyingine sitofikiria mara mbili nini cha kukufanya, ulistahili zaidi ya hapa” alisema kisha aligeuka aondoke lakini akapata hisia fulani iliyomwongoza kugeuka na kumtazama Mzee huyo aliyekua akitetemeka huku mara kadhaa akikodolea macho ndani.


Naye IGP akapeleka macho ndani ya Kijumba hicho, macho ya Elizabeth yakagongana na macho ya IGP Hassan Kitulo, lakini IGP alikua hajamwona Elizabeth ila macho yote aliyatupa kwenye viroba, akapiga hatua dhaifu kuelekea mlangoni, aliyakaza macho yake, kisha alipapasa kiunoni pake akatoa Bastola. 


Endelea 


SEHEMU YA NANE


Naye Elizabeth akaiweka sawa Bastola yake baada ya kuona IGP alidhamiria kusogea mbele akiwa kimya. IGP hakukwepesha wala kupepesa kope za macho yake akiviangalia vile viroba, yule Mzee alipoona hivyo akaamua kumtoa IGP kwenye reli.


“Samahani kwa hilo, unajua hofu imetutanda sababu hatujui ni kitu gani kinafanyika hapa Kijijini” alisema yule Mzee, angalau aliweza kumfanya IGP amtazame yeye, haraka Elizabeth alihama eneo la viroba na kuingia chumbani.


“Unataka kufanya nini? Hebu ongoza ndani” alisema kwa kukaza sauti, IGP alisema tena kwa hasira wakati huo mmoja wa askari alifika hapo kumpa taarifa IGP


“Songa ndani haraka, angusha vile viroba” alisema akiwa amekaza sauti, hakuna kati yao aliyeweza kugundua kua Elizabeth alishahama haraka sana, Mke wa yule Mzee alijishika kichwa maana alishajua huo ndiyo mwisho wa Binti yao kama ambavyo Elizabeth aliwaahidi kama Polisi watamshtukia.


Yule Mzee alifika kwemye viroba wakati huo IGP akiwa ameielekeza Bastola yake vilivyo, moja ya sifa ya IGP Hassan Kitulo ni ulengaji, aliielekeza vyema Bastola yake, Mzee alipofika hapo alishusha pumzi kuu baada ya kukuta patupu, angalau alipata nguvu ya kufanya ambacho IGP alikua akikitaka


Aliviangusha kwa mbwembwe, palikua patupu hata IGP alishashusha Bastola yake na kuirejesha kiunoni


“Kuna nini?” alimgeukia yule Polisi aliyefika hapo, alimtazama kwa makini


“Hajapatikana popote ndani ya makazi haya” alisema, IGP akaitazama ile familia kisha akaondoka na yule Polisi aliyekuja. Wale wazee wakakimbilia chumbani, wakamkuta Elizabeth akiwa anachomoka chini ya Kitanda, akawakabidhi Binti yao Halafu akawaambia


“Ahsante kwa kunisaidia” alisema kisha aliketi kitandani, yule Mzee alimtazama Elizabeth, akiwa kama Mzazi alimtazama Msichana huyo kwa jicho la huruma sana, moyoni alijua hakua Mtu mbaya maana angelikua mbaya katu asingeli mshukuru Mzee huyo.


“Kwanini wanakutafuta kwa nguvu kubwa kiasi hiki Binti, huonekani kama Mtu mbaya” aliuliza kwa upole sana Mzee yule. Elizabeth aliingiza mkono wake kwenye chupi kisha alitoa Flashi ndogo akawaambia


“Wanaitafuta hii, kama nitakua salama hadi mwisho basi Rais atalazimika kuikimbia Nchi, anatumia nguvu kubwa kuhakikisha anaipata hii, ili waipate ni lazima waniuwe kwanza” alisema Elizabeth kisha aliirejesha ile Flashi mahali alipoitoa.


“Unataka tukupe msaada gani?” aliuliza Mzee yule tena aliuliza kama Mtu aliyeamua kutaka kumsaidia Elizabeth


“Nahitaji kutoka ndani ya Kijiji hiki nifike picha ya ndege, huko nitapata Msaada ninaoutaka, sioni kama mnaweza kunisaidia kwa lolote lile” alisema Elizabeth, yule Mzee alisimama kisha alielekea kwenye Begi moja akalisogeza pembeni, chini palikua na Mbao kadhaa fupi, akageuka kumtazama Ekizabeth kisha akaziondoa zile mbao


“Njoo” alimwita Elizabeth, haraka alisogea hapo, alichokiona alijikuta akimtazama zaidi Mzee huyo tena alimtazama kwa Mshangao, Elizabeth alichuchumaa ili kuangalia kwa ukaribu zaidi. Palikua na shimo dogo lililochimbwa na kusimikwa simenti, ndani yake palikua na Boksi lenye silaha nzito za moto


Pale pale Elizabeth alimnyooshea Bastola yule Mzee


“Wewe ni Nani?” alihoji Elizabeth.


“Usihamaki nataka kukusaidia kuondoka hapa Mwambisi” alisema yule Mzee kisha akamwambia


“Mimi ni mstaafu wa jeshi, hizi ni miongoni mwa silaha nilizozitunza kwa kipindi chote, nilikimbia Uwanja wa vita wakati wa vita ya kumwondoa Idi Amin, tangu hapo nimekua na hizi silaha, nazitumia kuwindia” alisema Mzee huyo, Elizabeth alimeza funda zito la mate kisha akapeleka mkono kwenye boksi hilo huku mate yakimtoka kwani alishajua kua silaha hizo ndizo zitakazo msaidia kuondoka hapo Mwambisi.


Palikua na M2 Carabaine, AK47 na Risasi za kutosha, alitabasamu.


 


**


Hekaheka Ikulu, simu ya dharura.


Simu ya Mezani ilikua ikiita mfululizo, Rais Lucas Mbelwa alikua kitini akionekana kukerwa zaidi na simu hiyo. Alikua ameloana jasho akiwa kwenye kiti kikubwa Ofisini kwake, shingo yake ndefu ilimeza mate mengi yaliyopita kwa shida sana, alilegeza tai yake huku akipepesa macho yake


Nywele zake alizozitia karikiti zilikua Tim-tim, pumzi nzito iliusindikiza mkono wake hadi kwenye simu ya Mezani, akaipokea kwa kuiweka sikioni moja kwa moja na kuanza kutupa maneno makali, halafu akamalizia


“Asipokamatwa tumeisha” alisema kisha aliikata simu hiyo, mara waliingia Wanaume wawili waliovalia suti nyeusi, waliketi bila kukaribishwa huku wakionekana kua na hali kama aliyonayo Rais Mbelwa, Mmoja aliitwa Ignas Zakaria, huyu alikua Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi, mwingine ni Balozi Juma Nguvumbili, huyu ni Balozi wa Tanzania Nchini Malaysia


“Tunafanya nini Mkuu, hali inazidi kua mbaya.


Tunaelekea siku nzima isiyo na mafanikio, huyu Kirusi ni tatizo kwetu” alisema Balozi Juma Nguvumbili akiwa anagonga meza, Rais Mbelwa alikua amejiinamia, hapo hapo Waziri Ignas Zakaria akatoa wazo


“Kama yupo ndani ya kile Kijiji basi hakuna budi kutuma kikosi kwa ajili ya kusafisha Kijiji chote, afie ndani yake” wazo la Waziri liliungwa mkono na Balozi ambaye alihanikiza


“Mkuu tuma kikosi kazi kwa ajili ya kusafisha kila kitu kule, IGP pekee apewe taarifa, hili tukio lifanywe kua ni ugaidi na tutapindisha maelezo ili picha kubwa iwe Ugaidi, japo Polisi wengi watauawa lakini kirusi kitakua kimeshaondoka” alisema, Rais alizisugua nywele zake alizozidi kuzitibua


Alhema kama vile anakimbizwa, macho yake yalikua mekundu shauri ya kutafakari kwa muda mrefu bila kupata jibu


“Vipi kuhusu wana Kijiji?” aliuliza Rais.


“Mkuu tunafyeka wote kisha kikosi kazi nacho kinafyekwa na kikosi maalum” alisema Balozi, haraka Rais bila kujiuliza mara mbili alinyanyua simu yake na kumpigia IGP Hassan Kitulo aondoke Kijijini hapo haraka sana Halafu akanyanyua simu kwenda kikosi fulani kwa ajili ya kufyeka kijiji kizima wakati huo huo alipiga simu ya dharura kule BLACK SITE na kuagiza Makomandoo kwa ajili ya kufyeka kikosi maalum ambacho kitafyeka Kijiji kizima. 


Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Tisa ya MSALA hapa KIJIWENI

Previous Post Next Post

نموذج الاتصال