MSALA Sehemu Ya Saba-07 |
MSALA Sehemu Ya Saba-07
MSALA
Ilipoishia “Huko nje vikosi viliwasili ili kumnasa Elizabeth, Rais aliagiza ni lazima anaswe au auawe. Namna vikosi vilivyojikusanya kwa ajili ya Msichana mdogo ilileta taswira halisi ya mambo mazito ambayo Elizabeth alikua nayo. Mkuu wa Majeshi ya Polisi IGP Hassan Kitulo aliwasili Kijjini Mwambisi kwa maagizo maalum ya Rais wa Tanzania Lucas Mbelwa.
IGP Hassan Kitulo akawatangazia Wanakijiji waliokimbilia majumbani mwao baada ya kuona Vikosi vya Polisi vikifika hapo.
Endelea
SEHEMU YA SABA
“Ndugu zangu wana Mwambisi, kama kuna Mtu amemwona Msichana mmoja mwembamba asiyetambulika hapa Kijijini atoe ushirikiano kabla Msako haujaanza kijijini pote. Ukigundulika utaingizwa kwenye Mkumbo” alisema IGP kwa kutumia spika maalum ili kila Mmoja apate kusikia, sauti ya Spika ilifika hadi ndani ya Kijumba cha nyasi alichojificha Elizabeth. Namna vikosi vilivyokizunguka Kijiji alitamhua fika kua hatoweza kuchomoka.
Ili apate Msaada alitakiwa kufika Picha ya ndege, huko angekutana na Mtu aliyezungumza naye kwa Njia ya simu.
“Asijaribu yeyote kutoka hapa, huo ni ujanja wao wala hakuna atakayeingizwa kwenye Mkumbo, mtakua salama” alisema Elizabeth huku akivalia nguo za Msichana aliyekua akiishi ndani ya Kijumba hicho, alijitanda vizuri kisha aliwaambia
“Naonekana kama Binti yenu si ndiyo, sasa mnatakiwa kunilinda—” kabla hajamaliza kuzungumza ilisikika sauti ya kugongwa kwa mlango wa nyumba hiyo, Askari wenye silaha walisambaa Kijijini hapo kuhakikisha Elizabeth ananaswa.
Nikiwa ninaning’inia, mlango ulifunguliwa, aliingia Mwanamke mmoja ambaye hakuficha sura yake, alisogea hadi karibu yangu akiwa ameshavuta stuli na kuketi, mkononi alikua ameshikilia picha. Alinionesha kisha aliniuliza
“Yuko wapi huyu Msichana?” kwanza nilimeza funda zito la mate lililoambatana na pumzi nzito ya moto, Mwanamke aliyeingia alikua mzuri sana, mwenye nywele ndefu zenye rangi ya kahawia
“Sijui alipo, mnanitesa kwasababu yake lakini sijui chochote kuhusu yeye” nilisema, yule Mwanamke alisimama
“Benjamin…” aliniita kwa jina langu tena kwa sauti ya upole sana, sijui alinijua vipi
“Najua wewe uhusiki naye, lakini niambie alikupa kiasi gani umsaidie kuitoroka Tanzania, wewe ni rubani na ulikua na safari Mchana wa leo kuelekea Abijan, alikuahidi nini?” aliniuliza, nikagundua Watu wale walifanya upelelezi wa kutosha wakagundua hadi safari yangu ya ndege ambayo nilitakiwa kuifanya Mchana wa siku ya leo
“Simjui yule Msichana, sijapata kumwona popote pale, sikujua kama kumsaidia alipokua anataka kuuawa ndiyo kumeniingiza huku, ninaapa simjui” nilisema, yule Mwanamke aliketi akiwa amevaalia koti jeusi, suruali nyeusi na kiatu kirefu cheusi.
“Naamini wewe ni Mzalendo Benjamin, uko tayari kuona Nchi yako ikichafuka kwa sababu ya yule Msichana ambaye umemsaidia kujificha?” aliniuliza yule Mwanamke, namna alivyoniuliza niliona palikua na sababu ya Mimi kutaka kumjua yule Msichana ni Nani haswa, ninachojua kuhusu yeye ni jina lake pia aliniambia ni Mchepuko wa Rais
“Kwanini mnamtafuta, ni Nani yule” nilimuuliza nikiwa bado naning’inia kwenye mnyororo uliofungwa eneo langu la mgongo.
“Hupaswi kuniuliza chochote bali unapaswa kujibu maswali ninayokuuliza Benjamin, huwezi kumsaidia Mtu ambaye humjui, sasa kama unafikiria nipo hapa kwa ajili ya kucheza Na wewe basi subiria wenye kazi ya kucheza na wewe” alisema kisha aliondoka na kuacha mlango wazi, wakaingia wanaume wawili walioficha sura zao wakiwa na Nyaya mikononi mwao.
**
Kijijini Mwambisi, jua la utosi.
“Shiii!!” alitoa ishara Elizabeth, akiwataka wasizungumze chochote kisha akawaambia
“Ahadi yangu iko pale pale, mkisema chochote nawauwa kama Kuku” alisema akiwa anaonyesha kwa vitendo namna atakavyowafanya kisha akamteka Mtoto wa kike wa Mzee mwenye nyumba, akamnyooshea Bastola
“Hii ndiyo dhamana yangu, Maisha ya Binti yenu yatabakia Mikononi mwangu hadi pale nitakapokua salama” alisema kisha alimsogeza yule Msichana hadi kwenye viloba vyenye vitu ndani, viroba vilikua karibu na ukuta, kwa namna vilivyosimama isingelikua rahisi kuonwa labda waamue kufanya upekuzi ndani, alizama hapo akiwa anajipa nafasi ya kuchunguza kwa kutumia upenyo mdogo ambao pia aliuelekeza mdomo wa Bastola kuelekea Mlangoni tayari kwa ajili ya kujitetea kama ingetokea ‘Ambushi’
Zilipita dakika mbili mlango ukiendelea kugongwa bila kufunguliwa, nje palikua na kikosi cha Askari sita huku taratibu wakiongezeka baada ya kuonekana Mlango unachelewa kufunguliwa, sasa uligongwa kwa nguvu kama unataka kubomolewa, vumbi likawatimkia walioko ndani na kuwafanya wakohoe, Mzee mwenye nyumba aliufungua mlango akiwa na fikra ya kitisho cha uhai wa Mtoto wake aliyetekwa nyara na Elizabeth.
Mzee huyo na Mke wake walikutana na macho makali na mustachi wa IGP Hassan Kitulo, aliyatoa macho kisha akawatupia swali kwa hasira
“Kwanini mmejifikiria kufungua mlango?” aliuliza hadi chembe za mate ziliruka, akameza funda zito la mate
“Hakuna jibu?” aliuliza akiwa ameshakunja ndita zake, palepale simu yake iliita, akaitoa mfukoni akiwa bado macho yake yapo kwa Wana familia hao
“Mkuu tunaendelea na upekuzi hapa Mwambisi, kuna viashiria kua alikimbilia hapa” alisema IGP baada ya kukaa kimya kwa dakika moja akisikiliza upande wa pili uliopiga simu hiyo, kisha alisikiliza tena na kutoa jibu
“Nimekuelewa Mkuu, hii ni operesheni inayoendeshwa kimbinu zaidi, nina hakika kabla ya jua kuzama atakua amepatikana” alisema tena, Elizabeth alikua akisikiliza akiwa pale ndani, baada ya simu kukatika IGP aliwatazama kwa hasira kisha akasema kwa nguvu
“Tawanyika” aliwaambia Askari waliopo pale kisha akabakia yeye peke yake, akamsogelea yule Mzee na kumtandika kofi.
“Siku nyingine sitofikiria mara mbili nini cha kukufanya, ulistahili zaidi ya hapa” alisema kisha aligeuka aondoke lakini akapata hisia fulani iliyomwongoza kugeuka na kumtazama Mzee huyo aliyekua akitetemeka huku mara kadhaa akikodolea macho ndani.
Naye IGP akapeleka macho ndani ya Kijumba hicho, macho ya Elizabeth yakagongana na macho ya IGP Hassan Kitulo, lakini IGP alikua hajamwona Elizabeth ila macho yote aliyatupa kwenye viroba, akapiga hatua dhaifu kuelekea mlangoni, aliyakaza macho yake, kisha alipapasa kiunoni pake akatoa Bastola.
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Nane ya MSALA hapa KIJIWENI