MSALA Sehemu Ya Nne-04 |
MSALA Sehemu Ya Nne-04
MSALA
Ilipoishia “Katikati ya Usiku, katikati ya Msitu, Baridi kali lilikua likinipiga, mvuke ulikua ukitoka mdomoni kila nilivyokua nikipumua. Mwili wangu wote ulijawa na tope zito linalonuka, wadudu nisiowafahamu waliupanda mwili wangu na kuanza kunipa Bugudhaa.
Mwanga mkali ulisogea hadi eneo la shimo nililopo, bado kichwa changu kilikua juu, sauti za Mbwa kubweka zilifika hadi eneo la juu la Shimo, haraka nilizamisha kichwa changu chote kwenye tope. Mbwa walibweka lakini wale jamaa hawakutaka kuamini kua ndani ya lile shimo lenye tope palikua na Mtu tena akiwa hai.
Endelea
SEHEMU YA NNE
Wakaondoka, niliponyanyua Kichwa changu ili nivute pumzi niligudua walishaondoka. Sasa wazo la Elizabeth la kunivua nguo zangu nililielewa baada ya wale jamaa kuziona zile nguo zikiwa chini ya Mti mmoja, akili zao zikawaambia kua tulikua tumeshakimbia umbali mrefu baada ya yale Mauwaji ya Wale wanaume sita.
Wakawashurutisha Mbwa wao kusonga mbele kutusaka, haikuchukua hata dakika moja Elizabeth alikuja, akanivuta juu kisha akauweka mkono wangu kwenye bega lake, akanisaidia kutembea tukibadilisha uelekeo, tuliukata Msitu taratibu maana nguvu zilishaniisha na yeye hakua na uwezo wa kuendelea kunisaidia
“Niache hapa, Okoa Maisha yako” nilimueleza Elizabeth.
“Hebu acha akili ya Kitoto, watakuuwa wale endapo watakunasa. Watakushurutisha hadi mwisho wa Uhai wako Benjamin” alisema Elizabeth
“Ilipofika siwezi kuendelea mbele Elizabeth, huwezi kuhatarisha Maisha yako kwa ajili yangu”
“Ulinisaidia, jukumu langu ni kuhakikisha nakuacha ukiwa salama pia. Kilomita chake kutoka hapa tutakua tumefika Barabarani” Niliposikia kua kilomita chache mbele tutakutana na Barabara nilipata nguvu ya Ghafla, basi tulizidi kusonga.
Kweli nilianza kusikia milio ya magari, ikanipa ishara zaidi kua Barabara iko karibu. Elizabeth alinisaidia kwa jasho na damu, kuna wakati niliona alikua amechoka lakini alihakikisha ananisaidia hadi tukafika Barabarani, nyuma yetu kwa zaidi ya Kilomita Nne tuliziona kwa Mbali gari zile zilizowaleta wale wanaume pale Msituni.
Bahati nzuri palitokea gari aina ya roli iliyokua imepakia Mbuzi, tulilipungia mkono ili litusaidie kutusogeza Dar-es-salaam. Wakatupatia msaada nyuma ya gari kwenye Mbuzi, ilikua ni ahueni kwetu sababu tulishaukimbia Msitu wa Umauti, Elizabeth alikua amevalia taiti na Top, Mimi nilikua na Boksa na singlendi vyote vilikua na tope zito jekundu
Elizabeth aliitafuta kamba ndani ya lile gari, akanifunga mahali nilipopigwa risasi, alikua na ujuzi wa mambo mengi yaliyozidi kunishangaza, baada ya kunifunga kamba nilijisikia poa kiasi hata kuweza kutembea mwemyewe japo kwa kujivuta tofauti na mwanzo.
“Ahsante kwa kusaidia Maisha yangu” nilimwambia Elizabeth akiwa amejiegesha mahali ameegamia gunia, hakusema chochote kile, nami nilijivuta na kuegamia gunia pia
“Kwangu huu mi Msala, sijui kwanini nilikusaidia Elizabeth” nilisema kwa sauti nzito iliyotoka kwa taratibu sana
“Sikia nikwambie kitu kimoja Benjamin, hayo yote unayoyazungumza hayawezi kutuweka sehemu salama, cha Msingi ni kuhakikisha tunafika sehemu salama kabla ya Mapambazuko” alisema Elizabeth, alionekana kua Mtu mwenye siri nyingi asiyependa kujadili mambo
“Nafikiri tumeshawakimbia, tumetoka kwenye ile hatari. Nafsi yangu inaniambia hili ni tukio ambalo sitokuja kulisahau katika Maisha yangu” nilisema huku nikitabasamu huku gari ikiwa inachanja mbuga kuelekea Dar-es-salaam.
“Benjamin hujui chochote, bado tupo kwenye hatari. Kama ni mpira basi hata kipindi cha kwanza hakijaisha” alisema Elizabeth, maneno yake yaliniudhi sana. Hakua Mtu anayeweza kumtia Mtu moyo
“Kwani wewe ni Nani, nimejiingiza chaka gani Mimi?” nilimuuliza kwa hasira.
“Nilikwambia Naitwa Elizabeth Mlacha, hilo ndilo jina langu halisi. Mimi ni Mchepuko wa Rais Lucas Mbelwa” kwanza nilishtuka eti yule Msichana ni Mchepuko wa Rais wa Tanzania. Nilijikuta nikicheka kwa maumivu, niliiyona dhihaka kubwa kutoka kwake
“Najua huwezi kuamini, lakini kaa ukijua kua Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo inayonitafuta. Haya ni maagizo ya Rais kua nikamatwe kisha niuawe” maelezo yake ya pili yalikatisha kile nilichokifikiria kua ni dhihaka, sura yake ilikua ikimaanisha anachokisema
“Kwanini Rais atake uuawe?” nilimuuliza.
“Utajua mbeleni, fahamu kua Wakikukamata hawatokuacha salama. Kupitia ile gari tuliyopata nayo ajali basi tarifa zako zimenaswa, wewe sasa ni miongoni mwa Watu wanaotafutwa kwa siri na Usalama wa Taifa” alizidi kusema maneno yaliyonitisha sana, sikujua ni kwanini alikua akitafutwa na Usalama wa Taifa na kwanini Rais aagize yeye auawe.
Hadi kufikia hapo nilikua na maswali mengi kuliko majibu, mwisho niliona alikua akisema maneno ya Uwongo, kwa jinsi nilivyozisikia simulizi za Usalama wa Taifa na namna walivyo makini isingelikua rahisi kwa yeye kuchomoka mikononi mwao Halafu hadi sasa hajanaswa.
Mara ile gari tuliyopanda ikaanza kupunguza mwendo kisha ikasimama kando ya Barabara, eneo lile lilikua giza tupu, Mimi na Elizabeth tulitazamana. Kabla hata hatujaulizana chochote alikuja Mtu mwenye Tochi kisha akasema
“Gari imechemsha inabidi tupate Maji ili tuendelee na safari, poleni sana” alisema yule Mtu, kisha aliondoka kabla hata hajatusikiliza tulitaka kusema nini, upepo mkali ulikua ukivuma. Sauti za kugongana kwa Galoni zilisikika kisha sauti za Makubhasi zikasikika zaidi zikitokomea, Watu wa kwenye lile gari ambao ni dereva na Msaidizi wake waliondoka
Haraka Elizabeth alishtuka, akanyanyuka kisha akaniambia
“Haiwezekani watuachie gari tena katikati ya Msitu, wanatuamini kiasi gani wakati hawatujui?” aliuliza, swali lake lilihitaji utulivu wa akili ili kupambanua mambo, lilikua na maana kubwa sana. Haraka vichwa vyetu vikaanza kuchakata taatifa ile, mara Elizabeth akachumpa hadi chini, sikuweza kukubali kuendelea kukaa ndani ya gari, nilijikokota na maumivu yangu nami nikashuka kwenye lile gari.
Palikua kimya hata sauti ya gari haikusikika, palikua giza kiasi kwamba ilikua ni lazima tupapasie ubavu wa gari. Elizabeth alikua ameshaufungua mlango wa mbele wa gari, bahati nzuri baada ya kupekua kidogo alikutana na tochi, akaiwasha na kuanza kulikagua gari
Hakuna alichokiambulia ndani ya gari, palionekana kua shwari sana
“Vipi unafikiria nini?” nilimuuliza huku nikisogea zaidi karibu yake
“Ninahisia mbaya kidogo japo haionekani kama wale Watu ni wabaya, kwanini watuache hapa?” naye aliniuliza, nilikuna kichwa changu kabla ya kumpa jibu
“Hata hivyo sisi siyo Watu wabaya kwao labda wametupa imani kwetu” jibu langu halikuonekana kumfurahisha sana Elizabeth, sote tuliketi chini tukisubiria Wale watu warudi ili tuendelee na safari yetu.
Dakika zilikatika, hakuna aliyekua na saa baina yetu. Tuliishi kwa kukisia kua ilikua ni karibu na mapambazuko japo bado anga lilikua jeusi.
“Mguu unajisikiaje sasa?” aliuliza Elizabeth huku akiushika mguu wangu wenye maumivu, ulivilia damu, ile baridi ilizidi kukoreza maumivu lakini nilikua na ujasiri wa kukabiliana nayo ili tutoke salama kwenye kisanga kile nisichokijua kilianzia wapi, nilijiinamia kabla ya kumtupia neno lenye kauli fupi yenye swali zito la Msingi
“Kwanini wanakutafuta?” Hali ya Mguu wangu haikua na faida kama kujua Elizabeth anayejiita Mchepuko wa Rais alifanya jambo gani linalomfanya atafutwe na usalama wa Taifa, japo sikua na uhakika kwa alichonieleza lakini niliamua kuyakubali maelezo yake
Akahamanika
“Ni mara ngapi nikwambie kua huu siyo wakati wa kukueleza kilicho sirini? Wewe ni Mwanaume wa namna gani usiyejua kusoma nyakati, kumbe napoteza muda kumsaidia Mtu mwoga kama wewe” alisema kwa hasira akinifokea, kisha sekunde chache baadaye alituliza munkali wake akasema tena kwa sauti ya upole
“Kama nitaanza kukueleza sasa basi Tutakamatwa kabla sijamaliza kukusimulia, ndiyo maana nataka tutoke salama kwanza kisha nitakueleza mbeleni, yawezekana kuna Mpango mwingine wa kunimaliza. Siyo kawaida eti hadi muda huu lisipite gari lolote katika Barabara hii” alisema Elizabeth kisha alinyanyuka na kuanza kuangalia huku na kule kama Dudumizi.
Mara tulisikia mchakacho kutokea Porini, Elizabeth akaiweka bastola yake sawa kwa ajili ya Usalama, mchakacho ulikua wa taratibu mithiri ya paka mwenye kuwinda, Mapigo yangu ya moyo yalianza riadha palepale
Kumbe walikua wale madereva wa Roli walikua wakirudi, Elizabeth aliwamulika tochi baada ya kusikia sauti zao. Alipogundua ni wao aliificha ile Bastola kiunoni, mmoja wa wale madereva aliingia moja kwa moja kwenye gari wakati yule mwingine akifungua Boneti ili aweke maji, Alivyofungua alikutana na nini? Usikose Msala Sehemu ya Tano hapa Kijiweni