MSALA Sehemu Ya Tano-05 |
MSALA Sehemu Ya Tano-05
MSALA
Ilipoishia “Mara tulisikia mchakacho kutokea Porini, Elizabeth akaiweka bastola yake sawa kwa ajili ya Usalama, mchakacho ulikua wa taratibu mithiri ya paka mwenye kuwinda, Mapigo yangu ya moyo yalianza riadha palepale
Kumbe walikua wale madereva wa Roli walikua wakirudi, Elizabeth aliwamulika tochi baada ya kusikia sauti zao. Alipogundua ni wao aliificha ile Bastola kiunoni, mmoja wa wale madereva aliingia moja kwa moja kwenye gari wakati yule mwingine akifungua Boneti ili aweke maji”
Endelea
SEHEMU YA TANO
Nilisali kwa Msalaba, angalau unafuu ndani yangu ulikua umepatikana, pumzi zangu zilitoka kwa nguvu huku mapigo ya moyo yakirudi kua sawa. Elizabeth alizunguka mbele ya gari ili kuona ambacho yule dereva alikua akikifanya, alimmulikia Tochi huku akimuuliza
“Mbona mmeenda bila tochi kwenye giza nene?” alihoji, yule dereva alianza kukosea kutia maji ya kupoza injini akajikuta akitetemeka.
“Kua Makini maji unayamaliza” alisema haraka Elizabeth.
“Kumbe mnapafahamu hapa, ni eneo gani hili Kaka?” Aliuliza tena Elizabeth, alijawa na udadisi, Mimi bado nilikua nimekaa chini nikidowea mazungumzo yao. Yule Mtu hakujibu chochote, Elizabeth akaanza kuinusa harufu ya hatari
Swali pekee alilojiuliza ndani ya kichwa chake ni kuhusu ukimya wa wale Watu, waliondoka wakiwa wanazungumza lakini walirudi wakiwa kimya, sasa Elizabeth akaanza kumkagua yule Mwanaume wa juu ya Boneti, alishtuka alichokiona. Macho yalimtoka pima
Kiuno cha yule Mwanaume kilikua na Bastola, haikuishia hapo kwa Elizabeth akawa anamsoma yule Mwanaume namna alivyokua akijiandaa kugeuka. Haraka Elizabeth akaiweka Bastola yake katika hali ya wepesi kuichomoa na kumshambulia, alichofikiria ndicho yule Mwanaume alichokua anataka kukifanya
Alipotaka kugeuka haraka,aliwahiwa na kupigwa risasi ya Kichwa, yule Dereva wa ndani ya gari akajibu mapigpo na kuanza kumshambulia Elizabeth ambaye alishalitambua hilo na kubonyea chini ya gari, milio ya risasi ilizidi kunipa kiwewe, niliketi pale pale nikiwa najiuliza nifanye nini.
Akili yangu ilisita kufanya maamuzi ya ama ninyanyuke au niendelee kuketi pale chini, nilipigwa na jiwe mgongoni kisha sauti ya kuniita kwa mbinje dhahifu niliisikia nikajua huyo atakua ni Elizabeth aliye upande wa pili wa gari, haraka nilijiburuza chini ya gari na kutokea upande wa pili nikakutana na Elizabeth
“Sikia Benjamin, hakuna aliye salama kwetu kuanzia sasa. Rais anafanya kila namna kutumaliza, hatupaswi kumwamini yeyote. Nataka tufike Dar lakini hatuwezi kuitumia Barabara” alisema kwa sauti ya chini akiwa amepiga magoti huku akiweka sawa nywele zake ndefu zilizo timka
“Vipi kuhusu aliye ndani ya gari?” nilimuuliza huku nikimeza mate yaliyojaa hofu, sauti yangu ilitoka kwa shida sababu pumzi niliyonayo ilikua ndogo sana kifuani.
“Ameshakufa, twen’zetu” alisema huku akiniinua, tukazama Msituni. Mita kadhaa mbele tulikutana na Miili miwili iliyo uchi ikiwa imetapakaa damu, Maana yake waliotushambulia hawakua wale madereva halisi walioenda kutafuta Maji bali ni Watu wanaotusaka kwa udi na uvumba.
“Unaona eeh, hata hapa Msituni siyo sehemu salama na mbaya zaidi sijui hapa ni wapi. Kama tumeshaivuka Chalinze basi tunahitaji utulivu wa mwili na akili, huko mbele hapafai” alisema Elizabeth, Msichana mdogo niliyemzidi parefu lakini alikua na maarifa ya Kijeshi hadi nilimwogopa. Nilitamani iwe ndoto ili niamke nisimulie ndoto niliyoiota lakaini haikua hivyo, ni Maisha halisi ndani ya Mkasa mzito wa ule Usiku ambao sitokuja kuusahau Maishani mwangu.
Riadha ya Moyo wangu ilizidi ukomo nikajikuta nalegea, katika Maisha yangu sikupata kuona maiti, wala Mauwaji kama Usiku ule. Damu zilikua zimetapakaa pale chini huku sisimizi wakiwa wanaizingira ile Miili ya wale Watu wasio na hatia yoyote ile, roho iliniuma
“Chukua Bastola, ukizubaa utafia hapa” alisema Elizabeth, ujasiri ambao alikua nao yule Msichana sikupata kuushuhudia popote zaidi ya kwenye filamu za kizungu, kama alikua akiigiza filamu ya Mapigano lakini hii ilikua na uhalisia wa Maisha.
Nikaibeba ile Bastola nikawa nauvuta Mguu wangu, tulitembea kwa muda mrefu, nilipochoka aliniweka begani na kunisaidia kusonga mbele, hakika ulikua usiku wa kutisha kwangu. Mapambazuko yalitukuta juu ya kilima kidogo hapo Msituni, hatukujua kama tulikua tunasonga mbele au tulikua tunazunguka tu Msituni.
“Inabidi niondoe hiyo risasi Mguuni vinginevyo Mguu utaoza” alisema Elizabeth, kweli damu ilikua imegandia pale Mguuni, risasi ilikua ndani ya Mguu wangu. Maumivu yake yalinipa homa ya ghafla, japo nilikua muoga lakini nilikubali risasi iondolewe Mguuni mwangu
“Itabidi unisubirie hapa, si unaona ule moshi pale mbele” alinionesha mahali palipokua pakifuka moshi, ilikua ni dalili ya uwepo wa Makazi ya Watu
“Naenda kule kutafuta Msaada wa haraka ili niitoe hiyo risasi, usitoke hapa Benjamin.” Alisema kisha akaiangalia Bastola yangu na kuiweka sawa
“Ukiona Mtu anataka kukudhuru unabonyeza hapa, hakikisha unamlenga ipasavyo” aliniambia akiwa anazifunga nywele zake vizuri, jua lilikua linaanza kutoka na kufanya Msitu utawaliwe na mwanga na mvuke, eneo ambalo sisi tulikuwepo lilitupa nafasi kubwa ya kuuona Msitu kwa kiasi kikubwa sana.
Elizabeth alikua na nywele ndefu kama za kisomali, pua yake ilikua imechongoka. Tope lilimganda vilivyo na kufanya kazi ya kumdadisi iwe ngumu lakini kwa muda mfupi niliomtazama niligundua alikua na weupe ulio fifia, sijui ulitokana na lile tope au ndiyo asili yake
Alikishusha kile kilima akiwa anakimbia, alikua na taiti pekee. Nilisubiria hapo ili atakaporudi aitoe risasi ndani ya mguu wangu wa kulia.
Alikifikia Kijiji, ndipo Moshi ulipokua ukifuka, tulikua tumeshafika Mlandizi kwenye Kijiji kimoja kinachoitwa Kitonga. Elizabeth alifika kwenye bwawa dogo na kujimwagia Maji ili kuondoa lile tope ambalo lingekua kituko kwake, akatafuta Duka la dawa kisha akaingia humo na kumweka chini ya ulinzi muuza dawa.
Akachukua alivyovitaka kisha alimpa onyo kali muuza Duka halafu akaondoka hapo haraka na kurudi Kilimani Msituni, alinikuta nikiwa nimejilaza. Alikua na mfuko wenye vitu vingi vya matibabu ikiwemo dawa na visu. Kitu cha kwanza aliniwekea dripu ya Damu maana nilivuja damu nyingi, japo yeye alikua na jeraha lakini aliona Mimi nahitaji matibabu zaidi yake.
Wakati damu inaingia aliifungua ile kamba, nilihisi maumivu makali sana kutokana na kuganda kwa damu kwenye kidonda, kisha alinitaka nivumilie nisipige kelele, alionekana kua na taaluma ya ugangaji, alijua nini anafanya hadi nilizidi kumshangaa, alinichoma sindano ya ganzi kisha alianza kazi ya kuondoa ile risasi
Maumivu niliyoyahisi sikupata kuwa nayo kabla ya hapo, maumivu yalisambaa mwili mzima wakati anaitoa ile risasi, akafanikiwa kuitoa na kuniacha na maumivu makali sana. Chozi lilinitoka, akaniweka dawa kisha akanifunga na Bandeji.
Nilizongwa na jinamizi la Usingizi nikiwa nimeegemea Mti mkubwa ulio juu ya kile kilima, kuondolewa kwa ile risasi kulinipa ahueni kubwa sana. Ndoto za ajabu zilinishika nikawa naweweseka, mkono wa Elizabeth ndio ulionigutua kutoka Ndotoni, jicho langu likakutana na komwe lake, kifua changu kilikua kinatoa na kuingiza hewa kwa kasi.
“Masaa manne umeyamaliza kwa kukoroma, Mwanaume halali Benjamin. Bado tupo Msitu wa Umauti” alinikumbusha Elizabeth akiwa ananitoa dripu ambayo ilikua imeshamaliza kazi ya kuniongezea damu. Kwa kiasi kikubwa nilijisikia vizuri
Nilikuta tayari ameniandalia Gongo la Mti kwa ajili ya kutembelea, nilitabasamu japo tulikua shidani lakini sikuacha kuusifu moyo wa Msichana yule nisiye mjua. Kabla hatujaanza kutoka tulisikia mlio wa Helkopta, macho yalimtoka pima Elizabeth, akasimama na kuanza kuifwatisha ile sauti huku akitazama juu
Akarudi mbio hadi mahali alipokua ameniacha
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Sita ya MSALA hapa KIJIWENI