MSALA Sehemu Ya Tatu-03

 

MSALA Sehemu Ya Tatu-03
MSALA Sehemu Ya Tatu-03

MSALA Sehemu Ya Tatu-03

MSALA

Ilipoishia “Nilifika mahali nikaamua kujificha maana tayari nilishachoka, nilijibanza nyuma ya Mti mmoja eneo ambalo lilikua limeshona miti midogo midogo iliyojitengeneza kama kichaka ndani ya Msitu huo, wale wanaume hawakuchukua dakika nyingi walifika nilipo huku wakiwa wanasema


“Kama hatutowapata basi tutakua tumejitoa kafara wenyewe” niliona wazi yule Msichana alikua Muhimu sana kwao, lakini sikuacha kujiuliza alikua ni Nani kwao, aliwafanya nini hadi watake kumuuwa. 


Endelea 


SEHEMU YA TATU 


Nilijinyanyua taratibu ili nirudi nilipotoka, yalikua mahesabu mazuri sababu wao walifikiria huwenda nilikua nimekimbia mbele zaidi, wakahamasishana kuzidi kwenda mbele, niliwachungulia na kuhakikisha walikua tayari wameshaondoka, nilihema kwa nguvu sababu nilizibana pumzi zangu kwa muda mrefu. Ilinihitaji umakini wa ziada maana pale Msituni ukigusa Majani au nyasi vibaya inakua kama unatuma ujumbe kua nipo hapa.


Taratibu nilijitahidi kutembea bila kupiga kelele zozote zile lakini ghafla nilisikia Mtu akiniambia


“Simama hivyo hivyo, jisalimishe” Moyo wangu ulipiga ghafla kisha ukasimama Ghafla kama Mtu aliyefariki, mkojo ukabisha hodi na taratibu bila kukusudia nilijikuta nikidondosha kojo lililoshuka kwenye suruali yangu, nilitetemeka kama nasikia baridi kali.


Kifo kilikua karibu sana kwangu, sikua na mahesabu sahihi ya pumzi zangu, kila kitu nilikiona kimesimama. Niliona huo ndiyo ulikua mwisho wangu ndani ya Msitu huo wa giza kali, lakini hapo hapo nilisikia sauti ya kishindo kikianguka chini, tochi ikatua chini kama imetupwa. Akili yangu ikaniambia kua Mtu aliye nyuma yangu alikua ameanguka chini ghafla, wakati huo upepo ulikua unaanza kuvuma pale Msituni.


Nilitamani kuongea chochote lakini nilikua katika hali ya woga iliyopitiliza sana, nikasikia sauti ya kike nyuma yangu ikisema


“Uko salama Kaka” sauti hiyo ilikua ni sauti ya Elizabeth, Msichana aliyenifanya nikaingia kwenye kisanga kizito, nilipata angalau nguvu ya kugeuka nyuma, alikua tayari ameshaiokota ile tochi na kuizima.


“Asante kwa Msaada wako Kaka yangu, bila wewe ningekua Marehemu sasa hivi. Sikuona sababu ya kukuacha ufe hapa, hawa Watu sio wazuri kabisa. Kilichobakia ni kuhakikisha tunatoka hapa Msituni salama” alisema kwa ujasiri sana kama siyo yeye akiyekua katika hali mbaya.


“Unajua kutumia Bastola?” aliniuliza, bado nilikua kwenye Butwaa zito la kujiuliza yule Msichana ni Nani, kwanini alikua akionekana kama Mwenye ujuzi fulani uliojificha?


“Hapana sijui kutumia” nilijibu.


“Usijali, unapaswa kujua kutumia Bastola. Huu ni msitu wa Umauti, ukizubaa utafia hapa” alisema Elizabeth kisha alinipatia Bastola


“Umepata wapi?”


“Nimeuwa Watu wawili wenye Bastola, jitahidi uitumie kujiokoa Kaka yangu” alisema Elizabeth, kiukweli sikua na chaguo zaidi ya kufwata maneno yake lakini kiukweli alinionesha waziwazi kua alikua ni Mtu mwenye mambo mengi ya siri na pengine ndiyo sababu ya kutaka kuuawa. Aliwezaje kupona kwa yale majeraha ilikua ni kizungumkuti kwangu.


“Wewe ni Nani?” nilimuuliza, kiu yangu ya kutaka kumjua ilikua juu zaidi, nisingeliweza kuongozana na Mtu anayenipa mashaka kila sekunde


“Kwanza tutoke hapa Msituni kisha utajua kila kitu, muhimu ni kuokoa Maisha yako” alisema, akaongoza mbele. Cha ajabu alikua amevalia suruali na siyo gauni tena, alizidi kunifanya nimtafakari kila hatua ambayo nilikuwa naipiga


Nililazimika kuishikilia ile Bastola, ilikua nzito. Ni mambo ambayo nilikua nayaona kwenye filamu lakini nilijikuta katika Mkasa mzito usiku ule, tochi zilikua zikiwaka kila kona, tulitembea kwa kujificha ficha


“Tunaenda wapi?” nilimuuliza maana sikuona dalili yoyote ya kutoka pale Msituni, kadili tulivyokua tukitembea niliona wazi tulikuwa tukienda mbali kabisa na kuzama zaidi Msituni


“Tunaokoa Maisha yetu, Kaka yangu huu siyo wakati wa maswali wakati kila kitu umekiona. Kama unataka kufa basi chagua njia yako, pengine hujajua wale watu ni akina Nani, utawajua mbeleni” alisema akiwa amesimama ananiangalia, namna alivyosema niliona wazi hakuhitaji nimdadisi tena, basi nilimeza mate nikapiga moyo konde ili safari izidi kusonga.


“Naitwa Benjamin Kingai” nilijitambulisha


“Tuokoe Maisha kwanza” alinijibu haraka, kisha alinitaka nibonyee chini, ghafla ukapita mwanga mkali sana, wale Wanaume waliamua kuja na taa kubwa zenye kumulika eneo kubwa la Msitu, operesheni ya kutusaka ilichukua sura mpya. Bahati nzuri hawakuweza kutupata na ule mwanga Mkali.


“Wanataka kunipoteza, katika mpango huu hawawezi kukuacha salama, kua Mkakamavu vinginevyo hautojulikana mahali ulipo” alisema Elizabeth, alinisaidia kuiandaa ile Bastola ili kazi yangu iwe kufyatua risasi tu.


Mara tulisikia Mlio wa mashine ambayo namna ilivyokua ikiunguruma ilionesha ilikua inafanya kazi nzito sana, nilichungulia. Kumbe mahali ambapo tulikuwepo palikua karibu na lile gari tulilopata nalo ajali, lilikua linavutwa na kupelekwa juu ya Barabara. Hii ikanifanya nigundue kua Waliokua wakimsaka Elizabeth walikua Watu wazito, swali langu lililojirudia kichwani nilijiuliza Elizabeth ni Mtu wa namna gani haswa.


Tofauti na mwanzo nilipofikiria huwenda alikua kahaba aliyekorofishana na wale jamaa ndiyo wakataka kumdhuru lakini matukio mapya yalinibadilisha mtazamo wangu kabisa.


“Unaona, ushahidi wa lile gari unaharibiwa, haitojulikana ulipata ajali. Lengo sasa ni kutufuta” alisema Elizabeth, nilizidi kuogopa hadi Masikio yangu yalinisimama. Niliweza kuwaona wale Wanaume waliokua wakitusaka


Wote walificha sura zao kwa kutumia Mask nyeusi, sikuweza kuitambua sura yoyote ile, walifanya mambo yao kimya kimya. Sasa sekunde chache mbele walianza kusogea eneo tulilokua tumejificha, Elizabeth akanitaka niweke vizuri Bastola yangu. Walikua Watu sita waliokuja eneo lile wakiwa na taa kubwa


Walisogea karibu nikawa natetemeka, ile hofu ikasababisha nikohoe, pale pale mmoja wao akapiga filimbi. Haraka Elizabeth akafyatua risasi za haraka haraka na kuwadondosha wote sita. Zikaanza kusikika filimbi nyingi zikija tulipo, Binafsi nilichanganikiwa sana


Elizabeth akachomoka nami nikachomoka nikawa namfwata kwa spidi kwa nyuma maana yeye ndiye aliyekua akiniongoza pale Msituni, Risasi zikawa zinatukosa lakini kwa Bahati mbaya nilipigwa risasi ya Mguu, pale pale nilianguka chini huku nikiwa na maumivu Makali sana, Haraka Elizabeth akarudi kunisomba na kunisaidia kusonga mbele huku Damu ikiwa inanivuja sana.


Alinivuta na kunikalisha chini nikiwa ninalia, sikuwahi kupata jelaha lililonipa maumivu makali kama jeraha lile la risasi, nilihisi kama Mguu wangu wa kulia ulikua unaning’inia kutokana na yale maumivu makali niliyokua nikiyapata, zile tochi zilizidi kusogea huku sauti za Mbwa zikiwa zinasikika zikija kwa spidi kubwa eneo ambalo tulikuwepo


“Vua nguo zako” alisema Elizabeth, yale maumivu yalinichanganya nikashindwa kumwelewa kwa haraka, nikamwona akinivua shati langu jeupe lililochafuka kwa matope kisha aliniondoa suruali yangu, halafu naye alivua haraka suruali na shati alilovaa kisha akazitupa zile nguo mita chache kutoka mahali nilipokua nimekaa nikiugulia maumivu


“Benjamin, hizi ni saa za mwisho. Kufa au kupona kutatokana na ujasiri, ulinisaidia hivyo siwezi kukuacha hapa najua watakumaliza. Nisikilize kwa makini, njia moja pekee iliyopo ni kuzama kwenye shimo lenye tope” aliniambia, namna alivyoongea alionekana kulifahamu vyema eneo lile, ni kweli palikua na mashimo yenye tope ambayo mara kadhaa nilitumbukia wakati namsaidia yeye alipo poteza fahamu


Pale karibu palikua na shimo lenye Tope, kwanza alizichukua Bastola zote akazificha kichakani haraka sana huku wale Mbwa wakizidi kuja kwa kasi ya ajabu, akanisogeza na kunizamisha kwenye shimo lenye tope


“Hakikisha unajificha vyema Benjamin, usikamatwe nitakurudia” alisema Kisha alikimbia, moyo wangu ulijawa na hofu kubwa sana. Nikawa nazama taratibu kwenye tope nikiwa nimeushikilia mzizi wa Mti maana bila hivyo ningezama mazima.


Katikati ya Usiku, katikati ya Msitu, Baridi kali lilikua likinipiga, mvuke ulikua ukitoka mdomoni kila nilivyokua nikipumua. Mwili wangu wote ulijawa na tope zito linalonuka, wadudu nisiowafahamu waliupanda mwili wangu na kuanza kunipa Bugudhaa.


Mwanga mkali ulisogea hadi eneo la shimo nililopo, bado kichwa changu kilikua juu, sauti za Mbwa kubweka zilifika hadi eneo la juu la Shimo, haraka nilizamisha kichwa changu chote kwenye tope. Mbwa walibweka lakini wale jamaa hawakutaka kuamini kua ndani ya lile shimo lenye tope palikua na Mtu tena akiwa hai. Mambo yanazidi kuwa magumu unadhani nini kitaendelea? Usikose SEHEMU YA NNE Ya MSALA Hapa Kijiweni

Previous Post Next Post

نموذج الاتصال